
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete, anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika Tamasha la Matumaini ambalo litafanyika keshokutwa Jumapili kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
Mratibu wa tamasha hilo, Abdallah Mrisho, amesema Rais Kikwete ambaye hivi karibuni alikuwa na ugeni mkubwa wa Rais wa Marekani, Barack Obama, amekubali kuwa mgeni rasmi ambapo atatoa neno la matumaini kwa maelfu ya watu watakaojitokeza uwanjani hapo.
Akizungumzia zaidi juu ya ugeni huo mkubwa, Mrisho alisema: “Rais Kikwete amekubali ombi letu la kuwa mgeni rasmi, atatumia nafasi hiyo kutoa neno la matumaini kwa wote watakaojitokeza uwanjani hapo.

“Rais pia ndiye atakayefungua mechi ya Wabunge wa Simba dhidi ya Yanga ambayo inasubiriwa kwa hamu kubwa. Kama ujuavyo rais wetu ni mtu wa watu na ni mpenda michezo, hilo linajulikana siku zote.”
Aidha, Mrisho aliongeza kwa kusema kuwa shabaha ya tamasha hilo ni kuamsha upya imani ya Watanzania kwa nchi yao. Kuwafanya wawe wazalendo na kila mmoja kujiona analo jukumu la kufanya, kuhakikisha Tanzania yetu inapiga hatua.
“Mbali na Rais Kikwete, wengine watakaotoa neno la matumaini siku hiyo ni Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe, Naibu Waziri wa Sayansi na Teknolojia, January Makamba na Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Global Publishers Ltd, Eric Shigongo.