Thursday, August 15, 2013

0

JERAHA LA SHEKHE PONDA BADO NI UTATA

Posted in
MADAI ya kupigwa risasi kwa Katibu wa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu Tanzania, Sheikh Ponda Issa Ponda yamechukua sura mpya huku daktari aliyeanza kumtibu akifichua siri nzito. Akizungumza na MTANZANIA katika mahojiano maalumu jana, daktari huyo anayefanya kazi katika hospital binafsi ya dini na ambaye hakupenda kutajwa jina lake gazetini, alisema tangu lilipotokea tukio hilo Agosti 10 mwaka huu, zimekuwapo taarifa ambazo si sahihi.
Kwa mujibu wa daktari huyo, baada ya Sheikh Ponda, kufikwa na mkasa huo aligomewa kupewa huduma katika Hospitali ya Mkoa wa Morogoro, na hivyo ikabidi apelekwe katika hospitali binafsi ya dini iliyopo Msamvu, ambako daktari huyo alimkuta na jeraha kubwa kwenye bega lake la kulia.

“Sheikh Ponda alipigwa na risasi kwani hata ukiangalia baada ya kufika na kumpatia huduma, kwanza jeraha linaonyesha ni risasi ambayo ilipigwa na kutokea upande wa pili.

“Na nilibaini kitu alichopigwa nacho Sheikh kinafanana na risasi ambayo alipigwa kwa mbele na kutokea nyuma… mimi na mwenzangu mmoja tuliweza kumpatia huduma ya kwanza kuzuia damu isiweze kuvuja sana.

“Baada ya hapo niliweza kuwasikia watu ambao walikuwa na Sheikh wakijadiliana wakisema kutokana na jeraha lake ni lazima waende Muhimbili au Agha Ghan ambako wangeweza kupata huduma kwa urahisi.



“Kikubwa nilichokifanya ni kutoa huduma ya kwanza ila tambua kuwa huduma kubwa ikiwamo ya kupasuliwa ilifanywa Hospitali ya Taifa Muhimbili. Ninashangaa ni kwa nini wana-taaluma wenzangu wamekuwa waoga kusema ukweli katika hili,” alisema daktari huyo.

MTANZANIA ilipotaka kupata ufafanuzi kuhusu jeraha hilo la Sheikh Ponda kama ni la risasi ama laa, Daktari huyo alisema uchunguzi wa awali alioufanya unaonyesha jeraha hilo ni la risasi.

Ofisa Uhusiano wa Hospitali ya Taifa Muhimbili, Aminieli Aligaesha alipotafutwa juzi na jana kutoa ufafanuzi wa jeraha hilo, hakuwa tayari kujibu swali hilo.
Aligaesha pia alitumiwa ujumbe uliosema hivi: “Kumekuwa na mkanganyiko juu ya jeraha la Sheikh Ponda. Madaktari wa MOI wanasema mfupa umevunja lakini wamempokea akitokea upande wa Hopitali ya Taifa Muhimbili. Je baada ya kufanyiwa matibabu ni nini walichobaini madaktari wa Muhimbili? Ni jeraha la risasi au ni nini?”

Pamoja na kutumiwa ujumbe huo, Aligaesha hakujibu chochote.
Katika mahojiano aliyofanya na gazeti la MTANZANIA Agosti 11 mwaka huu, Sheikh Ponda alisema polisi walidhamiria kumuua wapoteze ushahidi.

Alisisitiza kuwa jeraha lake limetokana na kupigwa risasi.

Sheikh Ponda alieleza kuwa alipigwa risasi na polisi wakati akiwa kwenye gari na wenzake. “ Nilimuona kwa macho yangu askari mmoja ambaye alikua amevaa sare akinilenga bunduki,” alisema.

Sheikh Ponda alisema anakumbuka baada ya kujeruhiwa alichukuliwa na pikipiki na kukuimbizwa katika Hospitali ya Mkoa wa Morogoro ambako hata hivyo hakuweza kupata matibabu.

“Baada ya kushindikana kupata matibabu katika hospitali hiyo ya mkoa nilipelekwa katika zahanati moja ya Msamvu ambako pia matibabu yalishindikana na ndipo nilipokimbizwa hadi katika Hospitali ya Muhimbili majira kama ya saa 9.00 usiku,” alisema.

0 Maoni/comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Msimamo Ligi Kuu TZ