HII NAYO BALAA: JINSI SHEKHE PONDA ALIVYOONDOLEWA HOSPITALI NA KUPELEKWA MAGEREZA
Posted in Shekhe Ponda
Wakili Nassor Jumaa anayesimamia Katibu wa Jumuiya na Taasisi za Kiislam nchini, Sheikh Ponda Issa Ponda (54) ambaye kwa sasa anakabiliwa na kesi mpya ya kufanya uchochezi katika maeneo mbalimbali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania amezungumzia leo hii majira ya saa 7 mchana nje ya viwanja vya Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam ambapo amesema kuwa amesikitishwa na hatua ya vyombo vya dola kumuondoa Sheikh Ponda aliyekuwa amelazwa katika wodi ya Kitengo cha Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Upasuaji wa Mishipa ya Fahamu (MOI) alikokuwa akipatiwa matibabu na kisha kumhamishia katika gereza la Segerea.
Wakili Jumaa amesema amesikitisha na kitendo hicho kwani muda mfupi baada ya wakili mwandamizi wa serikali Tumaini Kweka kumaliza kumsomea Sheikh Ponda shitaka linalomkabili, Hakimu Hellen Riwa alitoa amri ya kukaa chini ya ulinzi Sheikh Ponda aendelee na matibabu.
Jumaa akasema ameshangazwa kuona leo, wanausalama wamemtoa Sheikh Ponda wodini na kumpeleka katika gereza la Segerea na kwamba atalazimika kurudishwa tena mahakamani siku kesi yake itakapojatwa Agosti 28 mwaka huu, ambapo upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika.















