MDOGO WAKE WEMA SEPETU ASHINDWA KUINGIA TOP 5 MISS KILIMANJARO.
Posted in Miss Tanzania, Redds Miss Tanzania, Wema Sepetu
MREMBO, Winnie Shayo, amefanikiwa kutwaa taji la Redd’s Miss Hai 2013 katika shindano lililofanyika katika Hoteli ya Snow View iliyopo Bomang’ombe, mwishoni mwa wiki mjini hapa baada ya kuwashinda wenzake kumi akiwamo mdogo wa Wema Sepetu.
Nafasi ya pili ilichukuliwa na mshiriki Mary Chemponda huku nafasi ya tatu ikienda kwa Catherine Leonard.Warembo 10 waliokuwa wakiwania taji hilo katika shindano la kwanza la kufungua pazia kwa upande wa mashindano ya Mkoa wa Kilimanjaro, walipita jukwaani na vazi la ubunifu la jioni kisha kuhitimisha na vazi la ufukweni.
Winnie, ambaye ni mwanafunzi wa masomo ya uhasibu nchini Uganda, akizungumza na Tanzania Daima alisema nia yake ni kujiendeleza kimasomo, lakini bado ana mapenzi kwenye sekta ya ulimbwende na kusisitiza kuwa faraja anazopata kutoka kwenye familia hasa wazazi wake ndizo zilizofanya yeye kuingia kwenye shindano hilo.
Alisema amejisikia furaha baada ya kufanikiwa kushika nafasi hiyo na kwamba, anatamani kuwa mwakilishi mzuri wa mashindano yaliyoko mbele yake, yakiwemo ya ngazi ya mkoa, kanda na hatimaye taifa.
Shindano hilo lilisindikizwa na burudani kutoka kwa msanii wa muziki wa kizazi kipya, Rich Mavoko na kuhudhuriwa na mamia ya mashabiki wa urembo kutoka katika miji ya Moshi na Arusha, wengi wao wakiwa ni wafanyabiashara wa madini katika mji wa Mererani.
Warembo hao walipatikana kutoka vitongoji vya Kwa Sadala, Boma Ng’ombe, Sanya Juu, Machame na KIA, ambako miongoni mwao ni mdogo wa mrembo wa zamani wa Miss Tanzania 2006, Wema Sepetu, Weru Sepetu, ambaye hata hivyo hakufanikiwa kuingia hata tano bora.
Warembo wengine walioshiriki shindano hilo ni pamoja na Zena Ally na Ivony Steven ambao walifanikiwa kuingia hatua ya tano bora huku Sharon Abdallah, Julieth Kimaro, Rehema John na Modesta Joseph wakiishia hatua ya awali.
Shindano hilo limedhaminiwa na Kampuni ya Bia Tanzania (TBL), kupitia kinywaji chake cha Redd’s, Fem Security, Bonite bottlers, Snow View Hotel, Panone pamoja na migodi ya madini ya Anglo America Mining na Manga Germ.
chanzo:daima
0 Maoni/comments: