Saturday, October 12, 2013

0

HATMA YA WACHEZAJI WA SIMBA HENRY JOSEPH NA REDONDO

Hatma ya wachezaji Henry Joseph na Ramadhani Chombo
'Redondo' ambao wametemwa katika kambi ya Simba
inayojiandaa kwa mechi yao ya Ligi Kuu ya Bara dhidi ya
Prisons itajulikana leo wakati kocha wa timu hiyo Abdallah
Kibadeni atakapozungumza na wanahabari jijini Dar es Salaam.
Nyota hao wawili pamoja kiungo Abdallah Seseme na mabeki
wa pembeni, Issa Rashid 'Baba Ubaya' na Miraj Adam
hawatakuwapo katika mechi hiyo dhidi ya Prisons
itakayochezwa kesho kwenye Uwanja wa Taifa.
Afisa Habari wa Simba, Ezekiel Kamwaga aliiambia NIPASHE
jana kuwa Henry na Redondo ni baadhi ya wachezaji ambao
hawapo kwanye kambi yao na akisisitiza kwamba huo ni
utaratibu wa kawaida uliowekwa na klabu yao kwa nia ya
kuongeza morali kwa wachezaji.
Kamwaga alisema wachezaji wanaofanya vyema mazoezini na
katika mechi zilizotangulia ndiyo huitwa kuingia kambini kwa
mapendekezo ya mwalimu na kwamba pia klabu haiwezi
kuwaingiza kambini wachezaji wote 36 iliowasajili.
"Simba imesajili wachezaji 36, kambi inahitaji wachezaji 25 tu,
hivyo wanaofanya vyema na kuwaridhisha walimu ndiyo
huitwa kambini ni utaratibu wa siku zote tangu enzi za
Mfaransa Patrick Liewig, lakini sasa imekuwa kama ajabu,"
alisema.
Kamwaga alisema Baba Ubaya, Seseme na Miraj watakosa
mechi hiyo ya Prisons kwa vile ni majeruhi.
"Seseme na Miraji kama ilivyo kwa Baba Ubaya ni majeruhi
hivyo ni hakika hawatacheza mechi hiyo kama ilivyo kwa
wasioitwa kambini," alisema.
Mkutano huo wa Kibadeni na waandishi wa habari utafanyika
saa 5 asubuhi kwenye makao makuu ya klabu hiyo mtaa wa
Msimbazi, jijini Dar es Salaam.
Kibadeni alisema amelazimika kuitisha mkutano huo ili kuweka
mambo sawa na kufafanua baadhi ya taarifa ambazo amedai
zimekuwa zikichafua taswira ya kambi ya timu yao.
"Kutokana na hali ilivyo sasa, nimelazimika kuitisha mkutano ili
kuweka mambo sawa, baada ya hapo kila kitu kitakuwa
kikitolewa na msemaji wa klabu," alisema kocha huyo maarufu
kama 'King'.

0 Maoni/comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Msimamo Ligi Kuu TZ