Tuesday, October 22, 2013

0

GOLI LA HAMIS KIIZA LAUA MTU

GOLI la pili la Yanga lililofungwa
na mshambuliaji Mganda Hamis Kiiza
limedaiwa kusababisha kifo cha
shabiki wa Simba Ramadhani Mbande,
mkazi wa mtaa wa Matokeo kata ya
Mabibo, Kinondoni jijini Dar es
Salaam.
Mapema jana kulienea taarifa kuwa
mmoja wa mashabiki wa Simba (Mbande)
alipoteza maisha wakati kikosi cha
Yanga kinachonolewa na kocha
Mholanzi Ernie Brandts kilipokuwa
kikikifunga mabao mfululizo kikosi
cha Simba kinachonolewa na kocha
mzawa Abdallah Kibadeni 'King'
katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom
Tanzania Bara iliyomazika kwa sare
ya 3-3 kwenye Uwanja wa Taifa jijini
Dar es Salaam juzi.
Gumzo ilitinga Mabibo jana mchana na
kuzungumza na uongozi wa mtaa wa
Matokeo na familia ya marehemu
Mbande ambao walieleza kwa kina
kuhusu kifo hicho.
Mjumbe wa Shina Nambari 9 la Mtaa wa
Matokeo, ambako marehemu alikuwa
akiishi na familia yake, Abdul
Muganyizi alisema kuwa baada ya
Kiiza kuifungia Yanga goli la pili,
marehemu alipandwa na presha na
kuishiwa nguvu akiwa amekaa kwenye
kochi ndani ya nyumba yake
akifuatilia mchezo huo ulioingiza
Sh. milioni 500.727 zilizotokana na
viingilio vya washabiki 57,422
waliokata tiketi halali kuushuhudia.
"Mimi nilikuwa kwenye baa pale
jirani nikiangalia kupitia TV mchezo
dhidi ya watani wetu Simba,
tulipofungwa goli la kwanza huku timu
yetu (Yanga) ikionekana kuzidiwa,
nikaamua kukimbia kurudi nyumbani
maana nami huwa na presha.
Vijana wa Simba hapa mtaani wakawa
wananizomea. Kabla sijafika hata
nyumbani kwangu nikapata taarifa
kwamba jirani yangu Mbande amepatwa
na matatizo," alisema Muganyizi.
"Nilipofika nyumbani kwake nilielezwa
na mtoto wake mkubwa ambaye walikuwa
wakiangalia naye mpira kuwa baba
yake alipandwa na presha baada ya
Simba kufungwa goli la pili.
Kabla ya hapo alikuwa akiingia ndani
na kutoka kusaidia majirani ambao
walikuwa wakisukumana kuchota maji
kwenye bomba lake hapo nyumbani, si
unajua shida ya maji hapa Dar es
Salaam. Baada ya kuishia nguvu,
familia yake kwa kusaidiana na
majirani walimkimbiza hospitali
lakini tayari alikuwa ameshatangulia
mbele ya haki.
"Alikuwa na mke, watoto na wajukuu
na walihamia hapa (Mabibo) baada ya
serikali kubomoa nyumba za Magomeni
(Dar es Salaam) ambako alikuwa
akiishi na familia yake.
Nililazimika kufika nyumbani kwake
nikiwa kama mjumbe na jirani baada
ya kupata taarifa hizo, nikatafuta
sheikh na kuwatuma vijana wa mtaa
wetu kushughulikia masuala ya msiba.
Leo (jana) asubuhi ndugu zake
wamesafirisha mwili kwenda Morogoro
kwa ajili ya maziko," alisema zaidi
Muganyizi.
Hata hivyo, ndugu wa marehemu
walisema kifo cha marehemu kilitokana
na 'mipango ya Mungu' na hakina
uhusiano wa moja kwa moja na mchezo
wa watani wa jadi uliochezeshwa kwa
ustadi mkubwa na refa mwenye beji ya
Shirikisho la Kimataifa la Soka
(FIFA), Israel Nkongo.
"Sisi tunaamini siku za baba mdogo
(Mbande) zilikuwa zimefika kwa
sababu alikuwa anasumbuliwa na
maradhi ya presha kwa muda mrefu.
Watu wamekihusisha kifo chake na
mechi ya jana (juzi) kwa sababu tu
kimetokea siku ya mechi hiyo,"
alisema Aisha Salum wakati
akizungumza na mwandishi nyumbani
kwa marehemu Mbande.
Aisha aliendelea kueleza kuwa baada
ya kufika katika Hospitali ya Amana
iliyopo Ilala jijini Dar es Salaam,
madaktari walimpima baba yake na
kubaini kuwa tayari alikuwa
amefariki na kwamba mwili
ulihifadhiwa hospitalini hapo hadi
jana asubuhi uliposafirishwa kwenda
Morogoro kwa ajili ya maziko.
Jacob Ambwene (24), ambaye baba yake
Ambwene Nuaka alikuwa rafiki wa
marehemu, aliliambia gazeti hili
nyumbani kwa marehemu jana kuwa
usafirishaji wa mwili wa marehemu
ulianza majira ya saa moja asubuhi
na walitegemea kuzika jana jioni
mkoani Morogoro.
Katika mchezo huo wa juzi wa watani
wa jadi uliokuwa ukirushwa na
televisheni ya taifa (TBC1) kwa
kupitia udhamini wa Azam TV
walionunua haki za matangazo ya
televisheni ya ligi hiyo kwa Sh.
bilioni 5.6, Kiiza alifunga bao la
pili la Yanga akimalizia kwa mguu wa
kulia mpira wa kurushwa kama kona wa
mchezaji 'kiraka' Mrwanda asili ya
DRC, Mbuyu Twite dakika ya 36 ya
mchezo huo ulioanza saa 10:05
alasiri.
Kiiza, ambaye aliipa Yanga goli la
tatu katika dakika za majeruhi
kipindi cha kwanza, alifunga goli
pia katika mchezo wa mzunguko wa
pili wa ligi hiyo msimu uliopita
ambao Yanga ilishinda 2-0 dhidi ya
Simba Mei 18 kwenye uwanja huo wenye
uwezo wa kuketisha watazamaji
57,558.
Goli la kwanza la Yanga katika
mchezo wa juzi iliyoshuhudia magoli
manne yakifungwa na wachezaji wa
kigeni, lilifungwa na winga hatari
wa timu ya taifa (Taifa Stars),
Mrisho Ngasa katika robo saa ya
mchezo huo ulioweka rekodi ya sare
magoli 3-3 kila timu kumfunga,
mpinzani wake mabao matatu ndani ya
dakika 45 tangu timu hizo zianzishwe
miaka ya 1935 na 1936.
Simba, waliowanyang'anya Yanga
utawala wa mechi hiyo katika kipindi
cha pili na kurejesha magoli yote
matatu, walisawazisha kupitia kwa
mshambuliaji waliyemsajili msimu huu
akitokea klabu ya Daraja la Kwanza,
Pamba ya Mwanza, Betram Mwombeki
dakika ya 54, beki wa kati Mganda
Joseph Owino dakika mbili kabla ya
saa ya mchezo na beki mwingine wa
kati Mrundi Gilbert Kaze aliyefunga
kwa kichwa dakika tano kabla ya
filimbi ya mwisho ya refa Nkongo.
Wakati mchezo huo uliokuwa na ulinzi
mkali nje na ndani ya Uwanja wa
Taifa ukidaiwa kusababisha kifo cha
Mbande, katika hali isiyo ya
kawaida, zaidi ya washabiki 15
walianguka na kupoteza fahamu
uwanjani na kuwapa kazi ya ziada
watu wa msalaba mwekundu kuokoa
maisha yao

0 Maoni/comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Msimamo Ligi Kuu TZ