Jul
2013
04
TANZANIA YAENDA URUSI KUSHIRIKI MCHEZO WA RIADHA DUNIA
Posted in Riadha TanzaniaBendera ya Taifa la Tanzania inatarajiwa kupeperushwa katika mashindano ya dunia ya mchezo wa riadha, yanayofanyika nchini Urusi.
Chama cha Riadha Tanzania (RT) kinasema kwamba wanariadha wake wanajiandaa kwenda huko, baadhi wakiwa ni wale walioshiriki kwenye Michuano ya Olimpiki jijini London, Uingereza hivi karibuni.
Wanaobeba jina la Tanzania huko ni Mohamed Msenduki, Faustine Musa, Daudi Joseph na Zakia Mrisho ambao kwenye Olimpiki hawakuambulia medali.
Mashindano haya yanaanza Julai 10 na yataendelea hadi Julai 17, yakienda sambamba na michezo mingine. Hata hivyo, RT kama kawaida, wanasema hawana rasilimali fedha, hivyo wanawaomba wadau kujitolea kuwadhamini ili kufanikisha ushiriki wa wachezaji hao.
Katibu Mkuu wa RT, Suleiman Nyambui anasema kwamba mazoezi si tatizo kwa wanaridha hao, kwa vile wapo katika mazingira ya kupata mafunzo makazini mwao, hivyo isiwape shida wadau, kwa vile baadhi ni wanajeshi.
“Najua hii ni kama timu ya taifa inaenda huko kushiriki, hivyo ni vema ikahakikishiwa ushiriki wao unakuwa mzuri na kutuletea medali, sasa ili hayo yafanyike basi tuiunge mkono,” alisema Nyambui na kuongeza kwamba mara ya mwisho mashindano hayo kufanyika ilikuwa 2009 nchini Ujerumani.
0 Maoni/comments: