Jul
2013
04
TAARIFA TOKA CHANETA: MASHINDANO KLABU BINGWA NETIBOLI KUFANYIKA MBEYA
Posted in CHANETAWachezaji wa netiboli nchini Tanzania wanatarajiwa kupata changamoto kubwa, kwa sababu Klabu Bingwa ya Netiboli inaandaliwa mkoani Mbeya, na kila timu ingependa kulitwaa taji hilo.
Soka imekuwa ikipewa kipaumbele na wadau wengi wa michezo, lakini sasa lazima kugeukia michezo mingine ambayo kuna watu wanaoipenda, na pia baadhi ya wanamichezo wameonesha kuwa na uwezo nayo.
Chama cha Netiboli Tanzania (CHANETA) kinaandaa mashindano hayo kwa kushirikiana na Chama cha Netiboli mkoa wa Mbeya, ambapo mashindano yenyewe yatatikisa jiji la Mbeya kuanzia Agosti 24 hadi Septemba 7.
Kama ilivyo kwa klabu za soka zilizo kwenye pilika pilika za usajili, klabu za netiboli nazo zinaingia kwenye usajili wa wachezaji, na mwisho wa dirisha lenyewe ni mwisho wa mwezi Julai. Wanatakiwa kusajili wachezaji wa nje wasiozidi watatu.
Mashindano hayo, kwa mujibu wa Mwenyekiti wa CHANETA, Anna Kibira, yatakuwa jukwaa na fursa nzuri za kuiimarisha timu ya taifa, kwa kuangalia iwapo wachezaji waliopo wanafaa au waongezwe wengine watakaowika.
Kama ilivyokuwa kwenye wanariadha wanaokwenda Urusi, CHANETA inaomba wafadhili ili mashindano hayo yaende kama yalivyopangwa. Klabu nne za juu zitashiriki mashindano ya Ligi ya Muungano wa Tanzania, yaani Tanzania Bara na Zanzibar.
Timu za netiboli zinazowika nchini ni pamoja na JKT Mbweni, Jeshi Stars, Uhamiaji, Bandari, Filbert Bayi, Magereza Morogoro, RAS Lindi, Hamabe Mbeya.Magereza Dare s Salaam, Magereza Arusha, Magereza Mwanza, Magereza Mbeya, Mapinduzi Dodoma, Tamisemi, Tumaini na Temeke Queen.
0 Maoni/comments: