TFF yapinga ‘Mapinduzi’ Yanga!
Posted in TFF, Yanga SC
SHIRIKISHO la Soka Tanzania, TFF, limetangaza kutoutambaua uongozi wa muda uliowekwa madarakani na Wanachama wa Yanga.
Majuzi, zaidi ya wanachama 600 wa Yanga
wakiongozwa na Mwenyekiti wa Baraza la Vijana la Yanga, Bakili Makele,
pamoja na Mwenyekiti wa Baraza la Wazee, Ibrahim Akilimali, walitangaza
kumng’oa madarakani Mwenyekiti wao, Lloyd Nchunga.
Jana TFF imesambaza Taarifa
iliyosainiwa na Katibu Mkuu wake, Angetile Osiah, ikitaka Wananachama
wao kufuata Katiba zao zinavyosema kuhusu utaratibu mzima wa uongozi na
namna ya kuwaondoa viongozi wao madarakani.
Osiah alisema hakuna Katiba yoyote
inayomlinda kiongozi aendelee kukaa madarakani, lakini Klabu zinapaswa
kufuata utashi wa Katiba zao zinavyosema ili kufanya mabadiliko ya
uongozi ndani ya vyama vyao na si kupitia Vikao visivyo halali.
TFF imesema haiko tayari kufanya kazi
na uongozi wa Kamati za muda na imewaonya Wanachama wa TFF kuwa lazima
waheshimu Katiba zao katika kufikia maamuzi mbalimbali wanayofanya.
Kuhusu kujiuzulu Wajumbe wa Kamati ya
Utendaji wa Klabu hiyo, Osiah alifafanua kuwa Katiba ya Yanga inasema
wazi kuwa lazima nafasi za Wajumbe hao kujazwa kwenye Mkutano Mkuu wa
Klabu hiyo uliopangwa kufanyika Julai 15.
Tayari wajumbe saba kati ya 13 wa
Kamati ya Utendaji ya Yanga wamejiuzulu na mmoja, Theonist Rutashoborwa,
amefariki dunia Mwezi uliopita.
Wajumbe wa Kamati ya Utendaji ambao
hawajajiuzulu ni Mwenyekiti Nchunga, Sarah Ramadhani, Charles Mngodo,
Salum Rupia na Tito Ossoro.
0 Maoni/comments: