Friday, November 9, 2012

0

KUTOKA TFF NA WENZETU SOKAinBONGO.com>> RATIBA YAREKEBISHWA KUPISHA MECHI YA STARS

Posted in , , ,
>> UCHAGUZI TAREFA, TAFCA SASA DESEMBA 22
>> TFF YATOA PONGEZI KWA UONGOZI MPYA FA MWANZA
TFF_LOGO12Kamati ya Ligi ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania, TFF, imefanya mabadiliko madogo ya ratiba ya Ligi Kuu ya Vodacom, VPL, ili kupitisha Mechi ya Kirafiki ya Kalenda ya FIFA kati ya Taifa Stars na Kenya, Harambe Stars, itakayochezwa Novemba 14 Jijini Mwanza na mabadiliko mengine yanahusu Ratiba ya Ligi Daraja la Kwanza, FDL.
Zifuatazo ni Taarifa kamili za TFF:
Release No. 180
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Novemba 9, 2012
MECHI TANO VPL ZAPISHA TAIFA STARS
Kamati ya Ligi ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) imefanya mabadiliko madogo ya ratiba ya Ligi Kuu ya Vodacom ili kupitisha mechi ya kirafiki ya kalenda ya Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA) kati ya Taifa Stars na Kenya (Harambe Stars) itakayochezwa Novemba 14 mwaka huu jijini Mwanza.
Mechi tano za ligi hiyo zilizokuwa zichezwe Novemba 11 mwaka huu, zimerejeshwa nyuma kwa siku moja ambapo sasa zitafanyika Novemba 10 mwaka huu. Mechi hizo ni Simba vs Toto Africans (Uwanja wa Taifa), Kagera Sugar vs Polisi Morogoro (Uwanja wa Kaitaba) na Oljoro JKT vs Ruvu Shooting (Uwanja wa Kumbukumbu ya Sheikh Kaluta Amri Abeid).
Nyingine ni Tanzania Prisons vs JKT Ruvu (Uwanja wa Kumbukumbu ya Sokoine) na African Lyon vs Mtibwa Sugar (Azam Complex). Mechi ya Mgambo Shooting vs Azam (Azam Complex) yenyewe itachezwa Novemba 10 mwaka huu kama ilivyokuwa imepangwa.
Nayo mechi ya Coastal Union vs Yanga (Uwanja wa Mkwakwani) itabaki Novemba 11 mwaka huu kwa vile Novemba 10 mwaka huu uwanja huo utakuwa na mechi nyingine. TFF imepanga utaratibu wa kuwapata kwa wakati wachezaji wa Yanga walioitwa kwenye kikosi cha Taifa Stars.
Mabadiliko mengine ni ya Ligi Daraja la Kwanza (FDL) ambapo mechi ya Villa Squad vs Transit Camp iliyokuwa ichezwe Novemba 8 mwaka huu sasa inachezwa Novemba 9 mwaka huu, na ile ya Novemba 7 mwaka huu kati ya Burkina Faso na Small Kids inachezwa Novemba 9 mwaka huu. Viwanja ni vilevile.

Kamati ya Ligi imelazimika kufanya mabadiliko hayo kutokana na viwanja husika kuwa na mechi nyingine, na vilevile Small Kids kupata matatizo ya usafiri kutoka mkoani Rukwa kwenda Morogoro.
Boniface Wambura
Ofisa Habari
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)
Release No. 181
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Novemba 9, 2012
UCHAGUZI TAREFA, TAFCA SASA DESEMBA 22
Uchaguzi wa viongozi wa Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Tabora (TAREFA) na Chama cha Makocha wa Mpira wa Miguu Tanzania (TAFCA) sasa utafanyika Desemba 22 mwaka huu.
Kwa mujibu wa ratiba za uchaguzi za vyama hivyo, Kamati zao za uchaguzi zitatangaza kuanza mchakato wa uchaguzi Novemba 10 mwaka huu wakati fomu kwa wanaotaka kugombea uongozi zitaanza kutolewa Novemba 12 mwaka huu. Mwisho wa kuchukua na kurudisha fomu ni Novemba 16 mwaka huu.
Kamati ya Uchaguzi ya Shirkisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) imetoa mwongozo huo kwa Kamati ya Uchaguzi ya TAFCA baada ya kuomba hivyo kutokana na wagombea sita tu kujitokeza kuomba nafasi tatu za uongozi katika mchakato wa awali.
Kwa waombaji ambao awali walichukua na kulipia ada ya fomu za kugombea uongozi TAFCA na TAREFA, hawatatakiwa kulipia tena ada kwa nafasi zile zile walizoomba, isipokuwa watatakiwa kujaza fomu upya.
PONGEZI KWA UONGOZI MPYA FA MWANZA
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) linatoa pongezi kwa uongozi mpya wa Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Mwanza (MZFA) uliochaguliwa katika uchaguzi uliofanyika Novemba 8 mwaka huu.
Ushindi waliopata viongozi waliochaguliwa kuongoza chama hicho unaonesha jinsi wajumbe wa Mkutano Mkuu wa MZFA walivyo na imani kubwa kwao katika kusimamia mchezo huo katika Mkoa wa Mwanza.
TFF inaahidi kutoa ushirikiano wa kutosha kwa Kamati za Utendaji ya MZFA iliyochaguliwa chini ya uenyekiti wa Patrick Songora aliyechaguliwa kwa kipindi cha pili mfululizo.
Uongozi huo mpya wa MZFA una changamoto nyingi, kubwa ikiwa ni kuhakikisha unaendesha shughuli za mpira wa miguu kwa kuzingatia katiba ya chama chao pamoja na vyombo vya mpira wa miguu vilivyo juu yao.
Pia tunatoa pongezi kwa Kamati ya Uchaguzi ya MZFA na Kamati ya Uchaguzi ya TFF kwa kuhakikisha uchaguzi unaendeshwa kwa mujibu wa Kanuni za Uchaguzi za Wanachama wa TFF.
Viongozi waliochaguliwa kuongoza MZFA ni Patrick Songora (Mwenyekiti), Nassoro Mabrouk (Katibu) na Richard Kadutu (Mwakilishi wa Klabu TFF).
Boniface Wambura
Ofisa Habari
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)

0 Maoni/comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Msimamo Ligi Kuu TZ