Sep
2012
17
TAARIFA TOKA TFF LEO
Posted in TFF
IFUATAYO NI TAARIFA KAMILI KUTOKA TFF:
Release No. 147
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Septemba 17, 2012
UCHAGUZI WA WANACHAMA WA TFF

Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Njombe (NJOREFA)
Kamati ya Uchaguzi ya
TFF ilibaini kuwa uongozi wa muda wa NJOREFA haukutoa ushirikiano wa
kutosha kuiwezesha Kamati ya Uchaguzi ya NJOREFA kuanza mchakato wa
uchaguzi kwa tarehe kwa tarehe iliyokuwa imepangwa na hivyo kusababisha
kuchelewa kuanza kwa mchakato huo wa uchaguzi wa mkoa huo mpya.
Kamati imebaini pia
kuwa kutokana na changamoto za kiuongozi zinazoukabili mkoa huo mpya,
mchakato wa uchaguzi ulioanza Septemba 2, 2012 haukuzingatia kikamilifu
Kanuni za Uchaguzi za Wanachama wa TFF.
Kutokana na kasoro
hizo za msingi, mchakato wa uchaguzi wa NJOREFA utaanza upya Septemba
18, 2012 ukizingatia Kanuni za Uchaguzi za Wanachama wa TFF. Uchaguzi wa
NJOREFA utafanyika Oktoba 28, 2012.
Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Tabora (TAREFA)
Kamati ilibaini kuwa
kuna mkanganyiko katika mchakato wa uchaguzi wa TAREFA na kwamba
mkanganyiko uliotokea umesababishwa na Kamati ya Uchaguzi ya TAREFA
kutotimiza wajibu wake wa kusimamia uchaguzi wa TAREFA kwa mujibu wa
Kanuni za Uchaguzi za Wanachama wa TFF.
Kutokana na
kuvurugika kwa mchakato wa uchaguzi wa TAREFA uliosababishwa na kiwango
kikubwa cha ukiukwaji wa Kanuni za Uchaguzi, Kamati ya Uchaguzi ya TFF
imejiridhisha kuwa Kamati ya Uchaguzi ya TAREFA haina uwezo wa kusimamia
majukumu ya uchaguzi wa TAREFA na kuzingatia kikamilifu matakwa ya
Kanuni za Uchaguzi ya Wanachama wa TFF.
Kwa kuwa Kamati ya
Uchaguzi wa TAREFA imeshindwa kutimiza wajibu wake na hivyo kusababisha
mkanganyiko na uvurugaji wa uchaguzi wa TAREFA, Kamati ya Uchaguzi ya
TFF kwa mamlaka yake yaliyoainishwa katika Katiba ya TFF Ibara ya 49(1)
na Kanuni za Uchaguzi za Wanachama wa TFF Ibara ya 10(6), 26(2) na (3)
imeamua yafuatayo;
(i) Imefuta
Kamati ya Uchaguzi ya TAREFA. Uongozi wa TAREFA unatakiwa kuteua Kamati
mpya ya Uchaguzi itakayoandaa na kutekeleza majukumu yake ikizingatia
Kanuni za Uchaguzi za Wanachama wa TFF na Katiba ya TAREFA. Uteuzi wa
Kamati mpya ya Uchaguzi ya TAREFA ufanyike kabla ya Septemba 24, 2012.
(ii) Imefuta
mchakato wa uchaguzi wa TAREFA. Mchakato wa uchaguzi utaanza upya
Septemba 25, 2012 na uchaguzi utafanyika Novemba 4, 2012.
Vyama vya Mpira wa Miguu mikoa ya Manyara (MARFA) na Kilimanjaro (KRFA)
Uchaguzi wa MARFA na KRFA utafanyika Septemba 22, 2012 kama ilivyopangwa.
UTENDAJI WA KAMATI ZA UCHAGUZI ZA WANACHAMA WA TFF
Kamati imebaini
baadhi ya viongozi wa vyama vya wanachama wa TFF wanaomaliza muda wao
wanashiriki kudhoofisha michakato ya uchaguzi ya vyama vya mpira wa
miguu kwa kutotoa fursa kwa Kamati za Uchaguzi za vyama wanachama kuanza
michakato ya uchaguzi kwa tarehe zilizopangwa na Kamati ya Uchaguzi ya
TFF.
Kwa kuwa ni wajibu wa
viongozi waliopo madarakani kuhakikisha kuwa vyama vyao vinafanya
uchaguzi kwa mujibu wa Katiba zao na Kanuni za Uchaguzi, Kamati ya
Uchaguzi ya TFF haitasita kupendekeza kwa Mamlaka husika za TFF vyama
hivyo kuchukuliwa hatua za Kikatiba kwa kushindwa kutimiza matakwa ya
Katiba ya TFF kwa kuwa na uongozi ambao muda wa ukomo wa madaraka
utakuwa umepita na hivyo kutokidhi matakwa ya Ibara ya 12(2)(a) ya
Katiba ya TFF.
Kamati ya Uchaguzi ya
TFF inavishauri vyama wanachama wa TFF kuzingatia ratiba ya uchaguzi na
Kanuni za Uchaguzi za Wanachama wa TFF wakati wote wa michakato ya
uchaguzi wa viongozi wa vyama vyao. Viongozi walioko madarakani
wanatakiwa kutoa ushirikiano kwa Kamati za Uchaguzi kama ilivyoianishwa
kwenye Kanuni za Uchaguzi.
Hamidu Mbwezeleni
Makamu Mwenyekiti
Kamati ya Uchaguzi ya TFF
SOKA IN BONGO >>MAIN SOURCE
0 Maoni/comments: