MTUKUTU BALLOTELI AISHTAKI MAN-CITY
Posted in Manchester City, Mario Balloteli
Kutoka SokaInBongo.com
Straika wa Manchester City, mwenye
vituko bwelele, Mario Balotelli, ameamua kuifikisha Klabu yake mbele ya
Baraza Maalum la Ligi Kuu England akipinga kupigwa Faini ya Mshahara wa
Wiki mbili kwa rekodi yake mbovu ya utovu wake wa Nidhamu.

Mara baada ya Balotelli kutwangwa Faini
na Man City alikata Rufaa mbele ya Jopo Huru la Klabu hiyo lakini Rufaa
yake ilitupiliwa mbali na sasa ameamua kufikisha Rufaa yake kwenye
Baraza Maalum la Ligi Kuu England.
Balotelli anatarajiwa kuwepo mwenyewe
kwenye Rufaa yake mbele ya Baraza hilo akitetewa na Mwanasheria wake
kutoka Italy pamoja na Mwakilishi wa PFA [Professional Footballers'
Association], Chama cha Wachezaji wa Kulipwa.
+++++++++++++++++++++
VIFUNGO vya BALOTELLI 2011/12:
-v Dynamo Kiev (Machi 2011): Alitolewa nje kwa Rafu mbaya dhidi ya Goran Popov. Alifungiwa Mechi 4 za UEFA CHAMPIONZ LIGI.
-v Spurs (Januari 2012): Alifungiwa Mechi 4 na FA baada ya kumtimba Scott Parker bila Refa kuona.
-v Arsenal (Aprili 2012): Alitolewa nje baada ya kulambwa Kadi za Njano mbili ikiwemo Rafu mbaya kwa Alex Song. Alifungiwa Mechi 3.
+++++++++++++++++++++
Rufaa hii ya Balotelli inashangaza maana
Klabu zinaruhusiwa kumpiga Faini Mchezaji wake hadi kufikia Mishahara
ya Wiki mbili lakini zaidi ya hapo inabidi wapeleke Kesi kwa Baraza
Maalum la Ligi Kuu England ili wapewe Kibali.
Hatua hii ya Balotelli pia inastajabisha
maana kawaida Klabu na Mchezaji wake humalizana wenyewe ndani ya Klabu
yao lakini Kesi hii, ambayo Man City waliifungua tangu Aprili 2012,
imeshindikana licha ya PFA kujaribu kuisuluhisha.
Katika kipindi hicho kilichotajwa cha utovu wa Nidhamu wa Balotelli alipewa jumla ya Kadi za Njano 9 na Kadi Nyekundu 3.
Katika Mechi yake ya mwisho na Man City,
Balotelli alitolewa mapema Kipindi cha Pili wakati Man City
walipochapwa 3-2 na Man United hapo Desemba 9 Uwanjani Etihad na Mechi
iliyofuatia, juzi Jumamosi, Man City walipoifunga 3-1 Newcastle,
Balotelli hakuwemo kabisa kwenye Kikosi.
Mara baada ya Mechi hiyo na Newcastle,
Meneja wa Man City Roberto Mancini alisema: “Wakati huu, Mario hayupo
kwenye fomu nzuri na ndio maana yuko nyumbani. Ni sababu hiyo tu. Kurudi
tena kwenye Timu ni lazima afanye bidii mazoezini na akichezeshwa
lazima acheze vizuri.”
0 Maoni/comments: