TAARIFA TOKA TFF:: Na Waandishi SokaInBongo.com
Posted in TFF
>>KUONDOA CHEO "Makamu wa Pili wa TFF", KUUNDA "Kamati ya Rufaa ya Uchaguzi"
Shirikisho
la Soka Tanzania, TFF, leo, kupitia Kamati ya Sheria, Maadili na Hadhi
za Wachezaji, wamesambaza Taarifa iliyosainiwa na Mwenyekiti wa Kamati
hiyo, Alex Mgongolwa, ikielezea michakato ya kurekebisha Katiba yake
kama ilivoagizwa na CAF na FIFA.
IFUATAYO ni TAARIFA KAMILI:
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
17 Novemba 2012
Katika kikao chake cha tarehe 3 Novemba
2012, Kamati ya Utendaji ya TFF ilipokea taarifa ya mapendekezo ya
marekebisho ya Katiba TFF kama ifuatavyo:
1. Kuingiza kipengele kinachohusu
“Club Lincencing” kama ilivyoagizwa na CAF katika waraka wake unaowataka
wanachama wote wa CAF, ikiwemo TFF, kuhakikisha kuwa kipengele hicho
kinaingizwa katika katiba zao.
2. Kutokana na ushauri na maagizo
ya FIFA, TFF inatakiwa kuunda wa Kamati ya Rufaa ya Uchanguzi
(“Elections Appeals Committee”) na kuondokana na utaratibu tulionao hivi
sasa ambao Kamati ya Rufaa (“Appeals Committee”) inajigeuza na kuwa
Kamati ya Rufaa ya Uchaguzi wakati wa mchakato wa uchaguzi wa TFF.
3. Kuindoa nafasi ya Makamu wa
Pili wa TFF pamoja na kutamka kuwa Wawakilishi wa klabu za Ligi Kuu
katika Kamati ya Utendaji watachaguliwa moja kwa moja na klabu zenyewe.
Hii inatokana na azimio la Mkutano Mkuu uliopita la kuruhusu uundwaji wa
chombo huru cha kusimamia Ligi Kuu na Ligi Daraja la Kwanza pamoja na
kupitishwa kwa Kanuni zinazokiongoza chombo hicho kama zilivyopendekezwa
na klabu za Ligi Kuu na kupitishwa na Kamati ya Utendaji.
Baada ya kutafakari mapendekezo hayo, Kamati ya Utendaji ya TFF iliamua kuwa:
1. Ipo haja ya kuifanyia marekebisho Katiba ya TFF kama iliyopendekezwa.
2. Kwa vile mapendekezo mawili
kati ya matatu ya ya marekebisho ya Katiba yana uhusiano na Uchaguzi
Mkuu wa TFF, ipo haja ya marekebisho hayo kufanyika kabla ya kutangazwa
kwa Mkutano Mkuu wa TFF na kuanza kwa mchakato wa Uchaguzi Mkuu wa TFF.
3. Aidha, kwa vile TFF haina uwezo
wa kuitisha mikutano mikuu miwili – Mkutano Mkuu Maalum kwa ajili ya
marekebisho ya Katiba ya TFF; na Mkutano Mkuu wa Uchaguzi – katika
kipindi kifupi kijacho, marekebisho ya Katiba yafanywe kwa njia ya
Waraka (“Circular Resolution”).
4. Waraka huo (“Circular
Resolution”) uwe umeshatayarishwa na Sekretariati ikishirikiana na
Mwenyekiti wa Kamati ya Sheria ifikapo tarehe 15 Novemba 2012 na
ukabidhiwe kwa Wajumbe wa Kamati ya Utendaji wanaowakilisha Kanda za TFF
ambao watahakikisha kuwa kila Mjumbe wa Mkutano Mkuu wa Kanda husika
anapata fursa ya kutoa ridhaa yake.
5. Zoezi la kupata ridhaa ya Wajumbe wa Mkutano Mkuu liwe limemalizika katika kipindi cha siku 21.
6. Kikao kinachofuata cha Kamati
ya Utendaji kitafanyika Jumamosi tarehe 15 Desemba 2012 kwa madhumuni ya
kupokea taarifa ya zoezi hili na kufanya matayarisho ya Mkutano Mkuu.
Katiba ya TFF inaelekeza kuwa taarifa ya Mkutano Mkuu itolewe kwa
wanachama wake angalau siku 60 (“notice period”) kabla ya Mkutano. Hivyo
Kamati ya utendaji inatarajia kuwa Mkutano Mkuu wa Uchaguzi utafanyika
Jumamosi na Jumapili ya tarehe 16 na 17 na Februari 2013.
Kamati ya Utendaji ya TFF inasisitiza
kuwa utaratibu huu umeamuliwa kutokana na TFF kutokuwa na uwezo wa
kifedha wa kutayarisha mikutano mikuu miwili katika kipindi kifupi
kijacho. Kinyume chake ni kuchelewa zaidi kufanyika kwa Mkutano Mkuu,
jambo ambalo hatuna budi kuliepuka.
Kamati ya Utendaji ya TFF inatarajia
kupata ushirikiano wa karibu kutoka kwa Wajumbe wa Mkutano Mkuu wa TFF
na wadau wa mpira wa miguu kwa jumla ili kufanikisha zoezi hili na
hatimaye kufanikisha Mkutano Mkuu wa Uchaguzi wa TFF.
Wenu Katika michezo,
Alex Mgongolwa
Mwenyekiti
KAMATI YA SHERIA, MAADILI NA HADHI ZA WACHEZAJI
0 Maoni/comments: